Watu 21 wameuawa hivi punde Jumapili Septemba 8 kwa kupigwa risasi na wanamgambo katika soko la Sennar, kusini mashariki mwa Sudani, siku moja baada ya viongozi wa nchi hiyo kukataa jeshi huru la kuwalinda raia.
Mtandao wa Madaktari wa Sudani, ambao umetangaza idadi ya vifo vya watu 21, pia umeripoti zaidi ya watu 70 waliojeruhiwa katika shambulio hili la Septemba 8 huko Sennar kusini mashariki mwa Sudani. Shambulio ambalo wanasema limetekelezwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), wanamgambo walio chini ya amri ya Jenerali Mohamed Hamdane Daglo, wanaopigana dhidi ya jeshi la Jenerali Abdel Fattah al-Burhane.
Sudani inakumbwa tangu mwezi Aprili 2023 na mzozo wa umwagaji damu kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF. Mzozo huo umesababisha makumi ya maelfu ya vifo na kusababisha moja ya migogoro mbaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Mnamo mwezi wa Agosti, shambulio la kijeshi lilisababisha vifo vya watu 80 katika eneo moja la jimbo hili, chanzo cha hospitali na mashahidi wameripoti.