MWANANCHI
Hatimaye Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko 13 kwenye Baraza la Mawaziri yaliyohusisha Mawaziri nane, Manaibu watano, wakiwamo wapya wawili, ikiwa ni siku mbili kabla ya kuanza kwa Bunge, na ndani ya saa 48 kama gazeti hili lilivyoripoti Ijumaa iliyopita.
Rais pia aliwaapisha mawaziri wote 13 akiwamo waziri mpya wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe ambaye alisababisha hafla hiyo kuchelewa kwa kuwa alikuwa akitokea Davos, Uswisi.
Mabadiliko hayo, yanayoweza kuwa ya mwisho kwa Rais Kikwete, yamefanyika ikiwa imesalia miezi sita kabla ya kuvunjwa kwa Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.
Rais amelazimika kufanya mabadiliko hayo baada ya mawaziri wawili, Profesa Anna Tibaijuka na Profesa Sospeter Muhongo, kuondoka kutokana na kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, ambayo pia imesababisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi kusimamishwa kazi, huku waziri wa zamani wa wizara hiyo, William Ngeleja akivuliwa uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, Kikwete amewaondoa mawaziri wawili wazoefu kutoka Ofisi ya Rais, Steven Wasira na Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, kuwapangia wizara nyingine, huku akimhamishia Dk Mary Nagu kwenye Ofisi ya Rais na Jenister Mhagama (Waziri Mkuu).
Akitangaza mabadiliko hayo jana, Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue alisema mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, ambaye alikuwa naibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuanzia mwaka 2012 hadi 2014 na ambaye hadi jana alikuwa naibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ameteuliwa kumrithi Profesa Muhongo kwenye wizara hiyo tata ya Nishati na Madini.
Simbachawene anakuwa waziri wa nne kushika wizara hiyo tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani na anaingia wakati Steven Masele, aliyekuwa naibu Waziri wa Nishati na Madini, akiwa amehamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano). Nafasi ya Masele imechukuliwa na mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage ambaye ameteuliwa kwa mara ya kwanza.
Sefue alisema mbunge wa Ismani, William Lukuvi, ambaye tangu mwaka 2010 amekuwa Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na Bunge), ameteuliwa kuziba nafasi ya Profesa Tibaijuka ya uwaziri wa Kazi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Sura nyingine ngeni kwenye baraza hilo, kwa mujibu wa Sefue, ni ya mbunge wa Same, Anne Kilango Malecela, mmoja wa wazungumzaji wakubwa bungeni, ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu.
Alisema aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama amepanda kuwa Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Lukuvi.
Nagu amehamia Uhusiano na Uratibu (Uwekezaji na Uwezeshaji) na Dk Harrison Mwakyembe anayehamia Afrika Mashariki (Uchukuzi).
Wengine ni mwanasiasa mkongwe, Steven Wasira aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo akitokea Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, wakati Samuel Sitta anakwenda Uchukuzi akitokea Wizara ya Afrika Mashariki.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Songambele, Kata ya Ilela Tarafa Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi, Richard Madirisha (31), ameuawa kikatili kwa kuchinjwa shingo na kutenganishwa na kiwiliwili na kisha kunyofolewa viungo vya mikono na miguu na sehemu za siri na kichwa chake na viungo hivyo kupikwa ndani ya safuria kama mboga.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari mauaji hayo ya kikatili na kutisha yalitokea jana saa 5.30 usiku nyumbani kwa marehemu.
Kidavashari alisema, siku hiyo ya tukio marehemu alikuwa amelala nyumbani kwake akiwa na mkewe Meklina Mussa na ghafla walitokea watu watano ambao hawafahamiki na kuvunja mlango na kuingia ndani ya nyumba. ambao waliodaiwa kuwa na mapanga waliingia chumbani kwa marehemu na kumlazisha mkewe ajifiche kwa kujifunika na shuka usoni.
Alisema baada ya mkewe kujifunika walianza kumchinja marehemu kwa kutumia panga huku mkewe akiwa anasikia jinsi marehemu akilia kwa uchungu.
Kidavashari alisema baada ya kumchinja walichukua kichwa na kukiweka kwenye safuria na maji na kukipika kwenye moto uliokuwa unawake nje ya nyumba ya marehemu.
Alisema kisha walirudi ndani na kunyofoa sehemu za siri, mikono na miguu na kuziweka kwenye safuria jingine kwenye moto na kutokomea kusikojulikana huku viungo hivyo vikiendelea kuchemka ndani ya safuria hizo.
Kidavashari alisema mke wa marehemu baada ya kuona watu hao wametokomea alitoka nje na kwenda kutoa taarifa kwa majirani ambao walifika kwenye eneo hilo na kukuta viongo hivyo vikiwa ninaendelea kuchemke kwenye safuria hizo huku kiwailiwili chake kikiwa ndani ya chumba chake.
NIPASHE
Wakala wa Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), umetangaza kuwa wakati wowote kuanzia sasa serikali itapunguza bei ya umeme baada ya gharama za mafuta kupungua katika soko la dunia.
Tanesco inauza ‘uniti’ moja ya umeme kwa Shilingi 306 na pia hutoza tozo la Shilingi 7,000 ambalo halina kuhojiwa wala kupingwa likidaiwa ni la kuendesha shughuli za Ewura, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na kodi ya VAT.
Kaimu Mkurugenzi wa Umeme wa Ewura, Godfrey Chibulunje, alitoa ufafanuzi huo baada ya viongozi hao kuwabana wataalamu hao na watendaji wa wakala huyo, Shirika la Umeme la Tanesco kueleza kwa nini hawashushi bei za umeme wakati mafuta yameshuka.
Aidha, Chibulunje alisema serikali ipo katika mchakato wa kupitia mwenendo wa kupungua kwa bei ya mafuta kwa lengo la kuangalia namna ya kuwapunguzia mzigo wananchi.
‘’Muda si mrefu wananchi wataona matokeo ya kuanguka kwa bei ya mafuta, tunachokifanya ni kupitia gharama ya ununuzi wa mafuta mazito na kiasi gani wananchi wanaweza kuondokana na mzigo wa kununua umeme:- Chibulunje.
NIPASHE
Mtuhumiwa wa wizi wa rediokoli ya kituo cha polisi cha Litembo wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma Bosko Ndunguru (40), amefariki akiwa mahabusi na kitanzi shingoni.
Mwili wake ulikuwa unaning’inia kwenye dari ya mahabusi kituo cha polisi Mbinga mjini akidaiwa ni baada ya kujinyonga kwa shati alilokuwa amelivaa hapo awali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela , alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1.00 asubuhi ambapo alidaiwa mwaka jana Ndunguru anatuhumiwa kuvunja kituo cha polisi cha Kijiji cha Litembo na kuiba redio koli ya kituo hicho na kutoroka lakini baadaye alikamatwa.
Alisema kabla ya kujiua ilidaiwa alilalamika kuwa jamaa zake hawampendi jambo ambalo liliwashangaza mahabusu wenzake.
NIPASHE
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeshauriwa kuwasilisha katika kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi hati ya dharura ya muswada wa sheria wa kudhibiti mitandao ya kijamii ikiwa ni njia mojawapo ya kudhibiti matumizi mabaya ya njia za mawasiliano.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar (UVCCM) , Naibu Katibu Mkuu Shaka Hamdu Shaka, alisema wakati umefika kwa serikali kuwasilisha muswada huo ili kuzuia matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Shaka alisema mageuzi ya teknolojia na ujio wa utandawazi kwa dunia ya tatu ikiwemo Zanzibar umezikuta wakati zikiwa hazijajitayarisha na ujio huo na kwa sababu hiyo hivi jamii inashuhudia ukiukwaji mkubwa wa maadili, mila na utamaduni wa kuheshimu utu, huku baadhi ya wamiliki na waendesha mitandao ya kijamii wakiwavunjia heshima wananchi.
“Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema uhuru bila ya utii ni ujinga na akasema pia uhuru usio na mipaka ni sawa na wendawazimu…kwa maana hiyo sithubutu kukandamiza uhuru wa maoni, ila ninachohimiza ni wajibu katika jamii inayoheshimu umoja, amani na upendo:-Shaka.
Alisema kutungwa kwa sheria hiyo ambayo itahusisha matumizi ya tovuti, umiliki na uendeshaji kutasaidia kuepusha jamii kuingia katika mifarakano inayosababisha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
HABARILEO
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimeanza utaratibu wa kuondoa msimu wa mitihani kwa kuweka mfumo wa kufanya mtihani kila mtahiniwa anapohitaji ambapo wanafunzi wanaweza kuomba mitihani kupitia tovuti.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Tolly Mbwete wakati wa mahafali ya 27 ya chuo hicho yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.
Alisema baadhi ya juhudi zimefanyika kuboresha zaidi mazingira ya kusomea katika chuo kikuu huria na kuzidi kuongeza ubora wa elimu inayotolewa pamoja na kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi.
Alisema chuo kimeongeza idadi ya mitihani (Odex) ambapo sasa mitihani yote katika kitivo cha sheria inaweza kupatikana katika mfumo huo.
“Idadi ya mitihani katika mfumo huo katika vitivo vingine vya taasisi ya elimu endelezi imekuwa ikiongezeka kila mwaka kutoka 28 mwaka 2012 hadi zaidi ya 160 mwaka 2014:–Mbwete.
MTANZANIA
Askofu msaidizi wa kanisa Katolki Jimbo kuu la Bukoba ,Mathodius Kilaini,amesema iwapo fedha alizogawiwa na mfanyabiashara James Rumegalila kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zitadhibitika ni chafu,atazirudisha.
Akizungumza katika mahojiano Kilaini alisema Rugemarila alimgawia milioni 80,5 na sehemu ya fedha hizo amekwishazitumia wakati kiasi kilichobaki amekiacha kwenye akaunti yake hadi uchunguzi utakapomalizika na kubaini fedha hizo ni safu ama chafu.
Alisema iwapo ripoti za uchunguzi zitaonyesha fedha hizo ni chafu,itakua ni changamoto kwake kwa sababu atalazimika kuanza kutafuta kiasi alichokitumia ili kukamilisha kiwango alichopewa ili amrudishie aliyempa.
“Yalipoanza maneno nilisitisha matumizi ya fedha hizo hadi mambo yawe wazi,kwa kweli hii ni changamoto kubwa kwangu lakini sitaacha wala kukata tama katika azma ya kuendeleza kanisa na jamii nikitumia misaada mbalimbali:-Kilaini.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook