Aliyekuwa Mgombea Ubunge jimbo la Singida Magharibi 2020, Mdau wa Mazingira na Kada wa Chama cha Mapinduzi April 17, 2024 amezindua kampeni ya kupanda miti mkoa mzima wa Singida aliyoiita SINGIDA MPYA YA KIJANI INAWEZEKANA ambapo kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wamepanda miti 460 shule ya Msingi Mulagwe iliyopo Kijiji cha Minyughe, wilaya ya Ikungi kumuunga mkono Mwanamazingira namba moja nchini Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika Utunzaji Mazingira kudhibiti mabadiliko ya Tabia nchi.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi akiwakilishwa na Mkuu Idara ya Mazingira wilaya humo Bwana Richard na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali na wananchi, ndugu Suphian amesema wazo la kampeni hiyo limetokana na mkoa wa Singida alipozaliwa kusemwa vibaya kwamba unaoongoza kwa ukame, hivyo anaamini kampeni hii italeta hamasa kubwa kwa wanafunzi na wana Singida wote na kuishi katika utamaduni wa kupanda miti zaidi kuliko kukata miti na kuigeuza Singida kuwa ya kijani.
Aidha kuhusu kuichagua Shule hiyo kuanza kampeni hiyo, Suphian amesema ni kwasababu ana historia nayo kwani yeye na familia yake ndiyo waliyotoa eneo hiyo bure kujengwa shule hiyo.
“Eneo la shule hii lisilopungua hekari 15 nililitoa bure mimi na familia yangu kama sehemu ya kuunga mkono Serikali kwenye Sekta ya elimu, na kipekee niishukuru Serikali kwa kuiita shule hii ” Mulagwe” kwani Mulagwe ni jina la babu yangu ambaye alikuwa Mtemi akiongoza Kata yote hii ya Minyughe wakati wa ukoloni.”
“Nyie wanafunzi najua mna ndoto za kuwa Rais Dkt Samia, Daktari, walimu, wanasheria na kadhalika, niwaambieni hamuwezi kutimiza ndoto hizo bila kutunza mazingira kwa kupanda miti kwani miti ni uhai, hufanya bongo zenu kufanya kazi vizuri na hivyo kufanya vema kwenye masomo”