Mke wa Rais wa zamani wa Gabon, Sylvia Bongo Ondimba, amefungwa katika gereza kuu la Libreville, Gabon.
Alikuwa chini ya kizuizi cha nyumbani tangu mapinduzi ya kijeshi mwishoni mwa Agosti, ambayo yalimshutumu kwa ubadhirifu wa fedha za umma.
Mnamo tarehe 28 Septemba, alishtakiwa rasmi kwa “utakatishaji fedha na kughushi” na hatimaye kuwekwa kizuizini kwa muda baada ya kuhojiwa kwa muda mrefu na hakimu.
Wakili wa Sylvia Bongo, Me Gisèle Eyue-Bekale, alipata kuahirishwa kwa siku kumi kwa kusikilizwa kwa hoja ya kuachiliwa kwake.
Haya yanajiri wakati uchunguzi wa kina wa madai ya ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma unaomhusisha Sylvia Bongo na mwanawe, Noureddin Bongo Valentin, ambaye tayari yuko rumande, pamoja na maafisa sita wakuu wa zamani wa baraza la mawaziri la rais, kwa mujibu wa vyanzo thabiti vya mahakama. .
Jeshi lililopindua utawala wa Rais Ali Bongo kufuatia shutuma za udanganyifu katika uchaguzi lilimshuku hadharani Mke wa Rais wa zamani na Noureddin kwa “kumdanganya” rais wa zamani, ambaye alipata madhara makubwa kutokana na kiharusi mwaka 2018, na kuwa viongozi “halisi” wa nchini kwa miaka mitano iliyopita.
Mapinduzi hayo yalitokea usiku wa Agosti 30, chini ya saa moja baada ya kutangazwa kwa Ali Bongo Ondimba kuchaguliwa tena. Jeshi lilitangaza “mwisho wa utawala,” na Jenerali Brice Oligui Nguema, kiongozi wa mapinduzi, alitangazwa rais wa Mpito siku mbili baadaye.