Balozi wa Tanzania nchini Austria Celestine Mushi amefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Mkata Wilayani Handeni Mkoani Tanga ambapo Polisi wamesema gari alilokuwemo limeungua sana hadi majivu.
Mushi aliteuliwa na Rais Samia Suluhu kuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria January mwaka huu na May 5, 2022 akawasilisha hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Austria, Alexander Van der Bellen.
RPC wa Tanga Henry Mwaibambe ameongea na Ayo TV kwa njia ya simu kuhusu ajali ya Balozi Mushi kabla ya Rais Samia kutuma salamu za rambirambi, Kamanda Mwaibambe alisema walikua kwenye utaratibu wa kupima mabaki ya mwili ili kujua kama kweli ni ya Balozi kutokana na kuungua sana kiasi cha kutotambulika kwa macho.
“Ilikuwa ni ajali ya magari mawili kugongana, gari dogo aina ya Toyota Crown Mtu mmoja alikuwa analiendesha na limeungua hadi majivu, baadhi ya Ndugu zake Balozi walikuja wanahisi kwamba ni Balozi, hilo gari kwenye usajili jina linaonesha ni la huyo Balozi kwahiyo ndio maana wanahisi hivyo, tusubiri uchunguzi wa Wataalamu utafanyika kwa haraka tutajua tu”