Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakishirikiana na Wataalamu kutoka Nchini Ireland na Bahrain, wamewafanyia Watoto 31 upasuaji wa mfumo wa mkojo na haja kubwa ambapo sita kati yao walizaliwa wakiwa na jinsia tata.
Kutokana na hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi ameshauri Wazazi kuona umuhimu wa kujifungulia kwenye vituo vya afya ili Watoto wakizaliwa waweze kufanyiwa uchunguzi wa kina na kugundulika mapema ili isaidie kutibiwa mapema “Jamii iache tabia ya kuwanyooshea Watoto vidole pale wanaponekana wanafanya tabia zisizo za kawaida badala yake wawalete hospitali ili wafanyiwe uchunguzi na kupatiwa msaada”
Naye Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Watoto MNH Dkt. Petronilla Ngila amesema Mtoto anaweza akazaliwa akaonekana kuwa na maumbile ya kiume lakini kwa ndani anaweza kuwa na homoni na endapo akiendelea kulelewa kama Mtoto wa kiume akifikia kipindi cha balehe ataanza kuingia kwenye siku zake kama mtoto wa kike.
Akizungumzia ukubwa wa tatizo Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo na Upandikizaji wa Figo Dkt. Gabriel Mtaturu amefafanua kuwa kati ya Watoto elfu tano wanaozaliwa mmoja ana jinsia tata na kati ya Watoto 300 wanaozaliwa mmoja anazaliwa akiwa na jinsia zilizoungana.
“Watoto waliofanyiwa upasuaji walikuwa katika makundi manne ambapo baadhi walikuwa na jinsia tata,wengine walikuwa na maumbile ya kike ila ndani walikuwa na maumbile ya kiume, mmoja alikuwa na sehemu mbili za kutolea haja ndogo na mwingine alikuwa wa kike ila hana sehemu za siri hivyo walimfanyia upasuaji rekebishi na kumtengenezea maumbile ya kike” #MillardAyoUPDATES