Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa Zanzibar Salhina Mwita Ameir amekifungua rasmi kikao kazi cha wadau wa Mpango wa kuzinusuru Kaya za Walengwa kinachofanyika Kisiwani Pemba.
Katika hotuba yake, amesisitiza kuwa utekelezaji wa mpango wa TASAF ni mhimili mkubwa katika kutekeleza miradi ya kitaifa ikiwemo Afya, Elimu na Miundombinu.
Katika kikao kazi hicho cha siku mbili kinachofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kisiwani Pemba, Naibu Katibu Mkuu Salhina pia ameeleza umuhimu wa mpango wa TASAF katika kuimarisha usalama na amani nchini.
“Kwa sababu ukiwawezesha wananchi, wakiwa katika hali nzuri, amani na usalama vinapatikana kwa urahisi kabisa. Na kama wananchi watakuwa katika hali ya dhiki na mahitaji mengine hawayapati, amani inaweza kuwa hatarini.” Amesema Naibu Katibu Mkuu Salhina.
Aidha Naibu Katibu Mkuu Salhina ameupongeza uongozi wa TASAF kwa kuratibu mafunzo hayo ambayo yatawajengea uwezo watekelezaji wa mpango, huku akiwataka washiriki kuyapa umuhimu mafunzo hayo ili wakayatumie vizuri maarifa na uzoefu wanayoyapata kwa manufaa ya mpango na taifa kwa ujumla.
“Fursa hii ya kupata uelewa leo, itatupa nguvu ya utekelezaji wa majukumu yetu katika miaka hii miwili ijayo, na ‘performance’ ikiongezeka, hiyo ndiyo ‘credit’ kwetu sisi na kwa taifa kwa ujumla, kwa hiyo niwasihi watendaji wenzangu tuwe makini kwenye mafunzo haya.” Amesema Naibu Katibu Mkuu
Hafla hiyo ya ufunguzi ilihudhuriwa pia na Maofisa Waandamizi kutoka TASAF, akiwemo Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Ukaguzi wa Ndani Ndugu Shedrack Mziray, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga. Katikahotuba yake ya kumkaribisha mgeni rasmi, alianza kwa kuishukuru Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kusaidia utekelezaji wa Mpango wa TASAF, na akaeleza maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango wa TASAF.
“Kwa sababu sasa hivi tuna walengwa milioni 1.3. Lakini bajeti ya mradi kuanzia sasa mpaka mwisho wa miaka miwili ya nyongeza tuliyonayo tunataka tukamilishe tukiwa na walengwa wasiozidi laki tisa. Kwa hiyo kuna walengwa takribani laki 4 ambao ni lazima tuwatathmini ili tuweze kuwatoa kwenye mpango. Vinginevyo bajeti haitatosha, hiyo ndiyo changamoto tuliyo nayo.” Amesema Ndugu Mziray.
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo kutoka TASAF Bi. Mercy Mandawa Mariki, amewaeleza washiriki hao lengo mahsusi la kuandaa kikao kazi hicho na utaratibu utakaotumika ili kuyafikia matarajio yanayokusudiwa.
“Tulipata taarifa kuwa kuna pengo mahali katika uelewa kuhusu utekelezaji wa mpango, tukaona ni vema tuandae kikao hiki cha siku mbili cha kujengeana uelewa kuhusu utaratibu wa utekelezaji shughuli za mpango. Lakini pia ni wajibu na majukumu yenu kama wadau katika kusimamia utekelezaji wa mpango.”