Kufuatia changamoto ya uelewa mdogo wa wananchi wa masuala ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini kumepelekea kuibuka kwa taasisi mbalimbali za kuisaidia serikali kukabiliana na changamoto hiyo.
Uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki zao, na njia za kufuata kupata haki hizo kumepelekea kuzinduliwa kwa taasisi ya Haki Maendeleo ambayo lengo lake ni kukuza uelewa wa wananchi na kufanya utetezi wa masuala ya haki za binadamu nchini.
Akiongea katika hafla ya uzinduzi wa taasisi hiyo pamoja na bodi yake ya wakurugenzi iliyofanyika leo (Februari 11, 2020), Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Haki Maedeleo,
Wilfred Warioba alisema kuwa njia nzuri ya kujenga uelewa wa wananchi ni kuwaelimisha na kuwashirikisha katika kufanya uamuzi wa maendeleo yao.
Alisema katika kufanya hivyo ni muhimu kukaa pamoja na viongozi wenye mamlaka kuwaelimisha umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika kutatua matatizo yanayowazunguka katika maeneo yao.
Ni muhimu kuwashirikisha wananchi katika kufanya maamuzi ya kujiletea maendeleo badala ya viongozi kuamua kwa niaba ya wananchi, maendeleo ya wananchi yaamuliwe kwa majadiliano, alisema Warioba.
Aliongeza kuwa kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya demokrasia, ni vyema pia kuwaelimisha watu kuhusu haki hiyo, hususani haki ya kushiriki katika kuchagua na kuchaguliwa.
Warioba alisema kuwa taasisi yake imelenga kutoa elimu ya haki za binadamu kupitia mawasiliano ya mifumo ya kompyuta, mitandao, simu za viganjani, michezo, vyombo vya habari, na muziki wa tamaduni ili kuchochea upelekaji wa ujumbe kwa urahisi kwa wananchi.
Awali akiongea, Mwenyekiti wa bodi wa Taasisi ya Haki Maendeleo, Dkt. Abdallah Mrindoko alisema kuwa kwa hali ilivyo serikali haiwezi kufanya kila kitu, hivyo taasisi kama Haki Maendeleo zinakuja kuisaidia serikali katika kutatua kero zinazowakabili wananchi wake.
“Katika jamii zetu bado kumekuwa na uelewa mdogo wa kujua haki na namna ya kuzipata, wananchi bado hawajajua mifumo sahihi ya kufuata ili kupata haki yake iliyopotea, wakati mwingine migogoro inatokana na hisia tu, lakini wananchi wakiwa na uelewa mpana itasaidia kupunguza migogoro” Mrindoko
Aliendelea kusema katika baadhi ya maeneo nchini kama vile Kilombero, Kilosa, Pwani kumekuwa na mogogoro mingi isiyokwisha ya masuala ya ardhi hivyo utatuzi wa hayo yote ni elimu kwa wananchi na upangaji mzuri wa matumizi bora ya ardhi.
Alisema taasisi ya Haki Maendeleo kwa sasa imeingia mkataba wa ushirikiano na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na itaendelea kushirikiana na wadau wengine ikiwemo serikali ili kuleta chachu ya maendeleo kwa wananchi.