Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Taasisi za Serikali kutumia njia mbalimbali bunifu ikiwa ni pamoja na kuanzisha hatifungani ya kupata fedha ili ziweze kugharamia miradi ya maendeleo kwa njia mbadala (APF) na kupunguza utegemezi kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.
Bashungwa ametoa wito huo Mei 15, 2024 jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa hatifungani ya kijani ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Tanga UWASA) kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Waziri Bashungwa ameeleza kuwa mkakati wa Hatifungani ya kijani ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2020/21 – 2029/2030 wenye lengo la kuhakikisha Taasisi na Ofisi mbalimbali za Serikali zinatumia vyanzo bunifu na mbadala katika kugharamia miradi ya maendeleo.
“Niwapongeze Wizara ya Maji kwa kuanzisha hatifungani katika miundombinu ya maji, na mimi nikitoka hapa nitakaa na wataalamu wa Sekta ya Ujenzi kuona namna ya kuiga wazo hili kwenye upande wa Sekta yetu”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amezisisitiza Taasisi na Mashirika mbalimbali kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kushiriki katika kikosi kazi cha kitaalamu cha kuangalia namna ya kuandaa Hatifungani ya Kijani ya kuwezesha kupata fedha za kutatua changamoto ya mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati hususan wanawake, vijana na makundi yenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Juma Aweso amezitaka Taasisi na Mamlaka nyingine za maji kujifunza kupitia Hatifungani ya Tanga UWASA kwani huo ni mlango muhimu katika kuleta maendeleo na mabadiliko kupitia Sekta ya maji ambayo inahusisha dhamira njema ya Rais Dkt. Samia Suluhu Haassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga UWASA, Mhandisi, Geofrey Hilly amesema kuwa chimbuko la wazo hilo liliibuka kwa ajili ya kutafuta fedha ili kuboresha miundombinu ya maji na chanzo cha maji katika jiji la Tanga amabapo lengo ni kuzalisha maji milioni 60 kutoka 45 wanayozalisha sasa.