Katibu Mkuu Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia Profesa Caroline Nombo ametoa wito kwa wanazuoni kuhakikisha wanatumia tafiti wanazofanya ili kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo katika jamii.
Profesa Nombo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili usimamizi wa masuala ya utafiti na Maendeleo kilichofanyika mkoani Morogoro
Amesema tafiti nyingi zimekua zikifanywa na wataalam pamoja na vyuo mbalimbali lakini tafiti hizo zimekua zikiwekwa kabatini badala ya kurejeshwa kwa wananchi .
Anasema kuwa upo umuhimu wa wataalamu kutoka vyuo vikuu na vituo vya tafiti nchini kukutana mara kwa mara ili kutafuta namna bora ya kuboresha mifumo ya ukusanyaji tafiti na kukumbushana namna ya kugawanya majukumu ili kupunguza mlolongo wa ukataji vibali vinavyo rasimisha ukusanyaji wa tafiti hizo.
Ukuaji wa sekta ya utafiti ni sawa na ukuaji wa nchi kiuchumi na kimaendeleo,katibu mkuu wizara ya elimu sayansi na teknolojia akiwa katika chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA Morogoro amekutana na wakuu wa taasisi na vyuo vikuu vinavyoendesha tafiti, kubwa hapa nikuweka mfumo imara wa ukusanyaji tafiti zenye tija kwa taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa sayansi teknolojia na ubunifu kutoka wizara ya elimu sayansi na teknolojia PROF,MAULILIO KIPANYULA- amesema kuna umuhimu kwa watafiti kutazama vipaumbele katika kufanya tafiti zao ili ziweze kuleta maendeleo endelevu nchini.
Naye makamu mkuu wa chuo kikuu cha sokoine cha kilimo SUA Profesa Raphael Chibunda amesema kuwa moja ya changamoto zinazowakabili watafiti ni uhaba wa fedha za kuendesha tafiti hizo kutoka Serikalini.
Amesema tafiti nyingi zinazofanywa na chuo hicho zinakua rafiki kwa wananchi kwani wanashirikishwa kuanzia mchakato wa awali hadi mwisho wa tafiti lengo kupata taarifa za uhakika na zenye uhalisia.