Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es salaam, Halima Bulembo ameziagiza Mamlaka za Serikali ikiwemo Wenyeviti wa Kata na Mitaa ya Kigamboni kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuwa maeneo yao ya biashara na wanayoishi ni machafu ikiwa ni sehemu ya tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu ambao umeripotiwa kwenye Mikoa kadhaa ukiwemo Mkoa jirani wa Morogoro hususani Wilaya ya Mvomero katika maeneo ya Tuliani na Dakawa.
DC Halima ametoa agizo hilo wakati yeye na Timu yake walipotembelea Mitaa mbalimbali ya Kigamboni ikiwemo maeneo ya feri na kufanya ukaguzi pamoja na kutoa elimu juu ya tahadhari ya ugonjwa huo.
“Tumekuja kutoa tahadhari kuna ugonjwa wa kipindupindu na kikifika hapa kwa mazingira yetu namna ambavyo hatufuatishi taratibu za usafi, tutashindwa kuendelea na kazi zetu kwasababu hatuwezi kuruhusu biashara ziendelee tukiwa tunapoteza Watu, tumekuja kutoa tahadhari kabla ya hatari”
“Maeneo ni machafu, tuishi na hii hali ya hewa lakini kwa kuzingatia usafi, kila mmoja awe Mlinzi wa mwingine, leo tumekuja kuwaomba kuzingatia usafi baadaye tutakuja kuwatangazia wanaoharisha na kutapika, ambaye atakaidi na kushindwa kufuata taratibu za usafi Vyombo vitamchukulia hatua, Wamama wengi tunazingatia usafi tunajua Wababa wanakuwaga na mambo mengi lakini tukiwashawishi watakuwepo”