Taiwan imefunga ofisi na shule na kusitisha safari za ndege huku kisiwa hicho kikikabiliana na kimbunga kikali ambacho kinatarajiwa kutua saa chache baada ya mafuriko ya Ufilipino.
Kimbunga Gaemi kinatabiriwa kupiga kaskazini mashariki mwa Taiwan saa 10 jioni (14:00 GMT) siku ya Jumatano, na Rais William Lai Ching-te alihimiza kila mtu “kutanguliza usalama” wakati wa mkutano wa dharura.
Mamlaka iliwahamisha zaidi ya watu 2,100 wanaoishi katika mazingira hatarishi katika mikoa mitatu ya kaskazini, hasa Hualien – eneo la milimani lenye hatari kubwa ya maporomoko ya ardhi.
Wizara ya Ulinzi ya Kitaifa ya Taiwan ilisema imewaweka wanajeshi 29,000 kusubiri kwa ajili ya juhudi za kutoa misaada.
Kimbunga hicho pia kilisababisha kufutwa kwa mazoezi ya kila mwaka ya jeshi la anga la Taiwan kwenye pwani yake ya mashariki na huduma za feri.
Takriban safari zote za ndege za ndani zilighairiwa pamoja na zaidi ya safari 200 za ndege za kimataifa, kulingana na Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano ya Taiwan.
Gaemi hakuanguka nchini Ufilipino, lakini aliimarisha mvua zake za msimu wa masika na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, na kuua watu wasiopungua 12 kufikia Jumatano, kulingana na wakala wa kitaifa wa kudhibiti majanga (NDRRMC) na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.