Takriban abiria 52 waliokuwa kwenye magari mawili ya uchukuzi wa umma wamekufa maji katika ajali iliyotokea kwenye jangwa magharibi mwa Niger, nchi iliyokumbwa na mafuriko tangu mwezi Juni, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Niger.
“Idadi ya muda inaonyesha watu 52 wamefariki na wengine kadhaa wametoweka,” limesema Shirika la Habari la Niger (ANP). “Niliona maiti 33” lakini “pia kulikuwa na walionusurika,” mwandishi wa habari wa eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP, ambaye ameongeza kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Tahoua (magharibi), kilomita 70 kutoka mji wa jina moja, kwenye barabara inayoliunganisha na eneo la Tillia, shirika hilo limesema. “Magari mawili yaliyokuwa yamebeba abiria wengi kwenda sokoni katika mji wa Tlemcess yalikwama kwenye kori (mfereji wa maji) kabla ya kuvamiwa na maji yaliyowasomba,” kimeeleza chanzo kingine cha eneo hilo.
“Operesheni ya kutafuta maiti na manusura wanaowezekana inaendelea (…) polisi na Walinzi wa kitaifa wana kazi ngumu,” ANP imesema, ikibainisha kuwa waathiriwa ni wafanyabiashara kutoka Niger na nchi jirani ya Nigeria. Mafuriko makubwa kutokana na msimu wa mvua tayari yamesababisha vifo vya angalau watu 94, zaidi ya waathiiriwa 137,000 na 93 kujeruhiwa kufikia Agosti 7, alitangaza Waziri wa Haki za Kibinadamu na Usimamizi wa Maafa wa Niger, Aïssa Lawan Wandarma.
Mikoa yote minane ya nchi – ikiwa ni pamoja na mji mkuu – imeathirika, hasa ile ya Maradi (kati-kusini), Zinder (kati-mashariki) na Tahoua (magharibi). Bado kulingana na waziri huyo, zaidi ya nyumba 15,000 na karibu madarasa arobaini yaliharibiwa. Zaidi ya ng’ombe 15,000 pia walisombwa katika nchi hii ambapo ufugaji wa mifugo ni moja ya nguzo kuu za uchumi.