Takriban bunduki 6,500 zilizokuwa zinamilikiwa kinyume cha sheria zimekabidhiwa kwa serikali ya Zambia baada ya serikali hiyo kuanzisha zoezi la kuwasamehe wanaomiliki silaha kinyume cha sheria nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa wa Zambia, Jack Mwiimbu amesema kuwa, bunduki hizo zimekabidhiwa kwa serikali ili ziharibiwe, ikiwa ni katika juhudi za Lusaka za kupunguza uhalifu na kuimarisha usalama nchini humo.
Waziri Mwiimbu amesema hayo Bungeni na kuongeza kuwa: “Tunawapongeza wananchi wote ambao wameitikia vyema mwito wa msamaha wa silaha na tunawaomba wengini nao wajitokeze zaidi kusalimisha silaha zao kwa Jeshi la Polisi la Zambia ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa.”
Amesema: “Serikali ina wasiwasi kuhusu matukio yaliyotokea hivi karibuni ya kufanyika mashambulizi ya silaha katika maeneo ya umma”
Ameongeza kwa kusema: Matumizi ya silaha na kumiliki bunduki kinyume cha sheria hakutaruhusiwa kwa mtu yeyote yule.