Takriban watu 170 “waliuawa” katika mashambulizi dhidi ya vijiji vitatu kaskazini mwa Burkina Faso wiki moja iliyopita, mwendesha mashitaka wa kikanda alisema katika taarifa yake siku ya Jumapili.
Aly Benjamin Coulibaly alisema mashambulizi hayo yalitekelezwa katika vijiji vya Komsilga, Nodin na Soroe katika jimbo la Yatenga mnamo Februari 25, na idadi ya muda ya “takriban watu 170 waliuawa”.
Uchunguzi umeanzishwa kuhusu mashambulizi ya watu wasiojulikana, aliongeza.
Taifa hilo la Sahel la Afrika Magharibi limekuwa likipambana kukabiliana na uasi ambao umeenea kutoka nchi jirani ya Mali katika muongo mmoja uliopita, na kuua maelfu ya watu na wengine zaidi ya milioni mbili kuyahama makaazi yao.