Jeshi la Israel lilisema Jumatatu linawahamisha takriban watu 100,000 kutoka mashariki mwa Rafah, kabla ya shambulio la ardhini linalotarajiwa katika mji wa kusini wa Gaza.
“Makadirio ni karibu watu 100,000,” msemaji wa jeshi aliwaambia waandishi wa habari alipoulizwa ni watu wangapi walikuwa wakihamishwa.
Watu waliambiwa wahamie Muwasi, eneo la kibinadamu lililotangazwa na Israel karibu na pwani. Jeshi hilo limesema limeongeza msaada katika eneo hilo, zikiwemo hospitali za shambani, mahema, chakula na maji.
Jeshi la Israel limeongeza kuwa operesheni yake ya kuanza kuwahamisha wakaazi wa Rafah mashariki ni ya muda na ni ndogo.
Afisa mkuu wa Hamas Sami Abu Zuhri aliiambia Reuters siku ya Jumatatu kwamba amri ya Israel ya kuhamishwa Rafah kabla ya mashambulizi yanayotarajiwa ni “kuongezeka kwa hatari ambako kutakuwa na madhara”.