Juhudi za uokoaji zinaendelea mashariki mwa Uganda kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyozika nyumba katika zaidi ya vijiji 6 wakati nyumba 45 zimezikwa kabisa.
Takriban watu 15 wakiwemo watoto 7 walifariki na wengine 113 hawajulikani walipo.
“Serikali sasa inanunua ardhi nyingine lakini unaona nini kimetokea, kwa hiyo, iwe hivyo sijui nitumie neno gani, lakini watu waondolewe eneo hili maana mvua zinaendelea kunyesha, unaona wote vilima, maji, maji yananyesha, mvua kubwa sana watu waondolewe mara moja na wito wangu kwa watu wa hapa tuhame na tukae na jamaa.
Maporomoko hayo yametokea baada ya mvua kubwa kunyesha usiku wa kuamkia leo katika eneo la milimani la Bulambuli. Wilaya hiyo iko takriban kilomita 280 mashariki mwa mji mkuu, Kampala.
Mwaka jana, wilaya hiyo tayari ilikumbwa na mvua za masika na kusababisha watu kupoteza maisha.
Polisi wa Uganda walisema kuwa wameimarisha shughuli za uokoaji pamoja na mashirika mengine dada ya usalama na kwa usaidizi wa jamii ya eneo hilo lakini wanazuiwa na barabara zisizopitika.
Boti mbili za uokoaji zilipinduka siku ya Jumatano wakati wa kazi ya uokoaji kwenye Mto Nile ambapo daraja la Pakwach lilizama.