Takriban watu 25 walikufa kwenye visiwa vya Comoro baada ya walanguzi wa watu kupindua mashua yao Ijumaa usiku, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM lilisema Jumatatu, tukio la tatu katika kipindi cha miezi mitatu.
“IOM Comoro ina huzuni kusikia kuhusu vifo vya watu wasiopungua 25 baada ya boti yao kupinduliwa kimakusudi na wasafirishaji kutoka Visiwa vya Comoro, kati ya Anjouan na Mayotte Ijumaa usiku,” IOM ilisema katika taarifa yake.
IOM, ikiwanukuu walionusurika, ilisema mashua hiyo ilikuwa imebeba takriban watu 30 kutoka mataifa tofauti, miongoni mwao wakiwa wanawake saba na watoto wanne.
“Manusura watano waliokolewa na wavuvi Jumamosi asubuhi,” IOM ilisema.
Mnamo Septemba, mashua iliyokuwa na watu 12 iliyokuwa ikisafiri kutoka Anjouan ilishindwa kufika Mayotte, wakati mwezi Agosti watu wanane walikufa katika tukio kama hilo, IOM ilisema, na kuongeza kuwa maelfu wamekufa kwenye njia hii tangu 2011 walipokuwa wakijaribu kufika Mayotte.