Takriban watu wanne wamefariki katika ghasia katika jimbo la kaskazini mwa India baada ya mamlaka kubomoa msikiti kwa madai kuwa ulijengwa kinyume cha sheria.
Ghasia zilizuka katika mji wa Uttarakhand wa Haldwani wakati wa kile polisi wanasema ni “hatua ya kupinga uvamizi”.
Mamlaka imesema kuwa zoezi hilo lilizinduliwa ili kusafisha majengo haramu, ikiwa ni pamoja na msikiti na madrassa (shule ya kidini) inayopakana nayo.
Waislamu walioswali msikitini wanasema wamekuwa wakilengwa isivyo haki.
Mamia ya waandamanaji na maafisa wa polisi walijeruhiwa katika mapigano hayo yaliyozuka Alhamisi jioni.
Video zilionyesha waandamanaji wakichoma moto magari na kuyarushia mawe na polisi wakiwarushia mabomu ya machozi.
Amri ya kutotoka nje imewekwa na serikali imetoa maagizo ya “kupiga risasi mara moja” ili kudhibiti hali hiyo.
Kisa hicho kilitokea katika eneo la Banbhoolpura huko Haldwani.
Wilaya hiyo ilishuhudia maandamano makubwa Januari mwaka jana baada ya zaidi ya watu 50,000, wengi wao wakiwa Waislamu, kupewa notisi ya kufukuzwa kwa madai ya kuishi eneo hilo kinyume cha sheria katika ardhi inayomilikiwa na Shirika la Reli la India.
Ubomoaji huo baadaye ulizuiliwa na mahakama kuu ya India.