Takriban watu sita wamefariki katika mlipuko uliolenga basi la abiria lililokuwa linasafiri katika mkoa nje ya mji mkuu wa Somalia Jumatano shirika la habari la serikali limesema.
Shirika la habari la Somalia limemnukuu Mohamed Ibrahim gavana wa Lower shabelle akisema kuwa shambulizi lilitokea katika barabara baina ya wilaya za Ooryoley na Marka na kwamba watu wengine 12 wamejeruhiwa.
Ibrahim amesema shambulizi la kigaidi limesababisha mlipuko , shirika hilo la habari limeandika katika mtandao wa X ambao awali ulikuwa unajulikana kama twitter.
Al-Shabab wenye mafungamano na Al Qaeda siku za nyuma wamechukua jukumu la mashambulizi kama hayo.
Kundi hilo limekuwa likipigana tangu mwaka 2006 kuiangusha serikali kuu ya Somalia na kuanzisha utawala wake kwa kuzingatia tafsiri kali ya sheria za Kiislamu.