Mafuriko makubwa yaliyokumba maeneo mbalimbali ya kaskazini mwa Sudan katika siku mbili zilizopita, yamesababisha vifo vya watu 31 na kubomoa mamia ya nyumba. Kwa mujibu wa msemaji wa Ulinzi wa Raia wa Sudan, Qureshi Hussein, mafuriko hayo yamesababisha uharibifu mkubwa katika jamii nyingi.
Mmoja wa wahanga, Yassin Abdul Wahab, alieleza jinsi alivyopoteza nyumba yake na kulazimika kujenga makazi ya muda kwa ajili ya familia yake. “Watu wanalala mitaani, na hali ni mbaya sana,” alisema, akiangazia hali ngumu wanayokabiliana nayo wakazi wa eneo hilo.
Mvua kubwa na mafuriko yaliyotokea Sudan mwezi huu yameathiri zaidi ya watu 317,000. Kati ya hao, watu 118,000 wamepoteza makazi yao, hali inayoongeza changamoto kwenye machafuko kutokana na vita vinavyoendelea nchini humo.
Tukio hili linakuja wakati Sudan ikiadhimisha siku 500 tangu nchi hiyo iingie kwenye vita baada ya mapigano kuzuka kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), hali inayoongeza mateso kwa raia.
Mamlaka za Sudan zinaendelea na juhudi za kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko, lakini hali ya ukosefu wa usalama inafanya juhudi hizi kuwa ngumu zaidi.