Wapiganaji wenye itikadi kali kaskazini mashariki mwa Nigeria wamewauwa takriban wanakijiji 37 katika mashambulio mawili tofauti, kwa mujibu wa wakaazi katika maeneo hayo.
Wapiganaji hao wenye itikadi kali waliwalenga wanakijiji katika wilaya ya Geidam katika jimbo la Yobe siku ya Jumatatu na Jumanne katika shambulio la kwanza katika jimbo hilo katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.
Awali watu hao wenye silaha waliwaua kwa risasi watu 17 kabla ya kuwaua wengine 20 kwa kutumia kilipuzi wakati wakihudhuria mazishi.
Kundi la Kiislamu la Boko Haram lilianzisha uasi kaskazini mashariki mwa Nigeria mwaka 2009 katika juhudi za kuanzisha matumzi ya kanuni zao katika eneo hilo.
Takriban watu 35,000 wameuawa na zaidi ya milioni 2 kukimbia makazi yao kutokana na ghasia katika jimbo la Borno, ambalo ni jirani na Yobe.
Rais wa Nigeria Bola Tinubu, ambaye aliingia madarakani mwezi Mei, hajafaulu kumaliza mizozo ya usalama katika taifa hilo katika maeneo ya kaskazini mashariki na kaskazini-magharibi na kati ambapo makumi ya makundi yenye silaha yamekuwa yakiua wanavijiji na kuwateka nyara wasafiri ili kuwalipa fidia.