Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Kigoma imebaini upotevu wa fedha Tsh. milioni 800 za mikopo ya 10% kutokana na vikundi vilivyoomba mikopo hiyo kutorejesha kabisa.
Akiongea na Ayo TV Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoani humo John Mgala amesema fedha hizo ni za Halmashauri za Kasulu, Kibondo, Kakonko, Buhigwe na Kigoma Ujiji na kuzitaka Halmashauri hizo kufungua kesi za Wadaiwa sugu.
Katika uchunguzi uliofanywa katika kipindi cha January hadi March mwaka huu Taasisi hiyo imebaini kuwa vikundi hivyo havifanyi shughuli ambazo wamekuwa wakiombea mikopo hiyo bali hugawana baada ya kuzipata pesa na hivyo kuwa vigumu katika marejeshi.
Watumishi watatu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji wanatajwa kuhusika katika mchakato wa upotevu wa fedha hizo ambao nao wanaendelea kufanyiwa uchunguzi.