ACHANA na pointi tatu ilizopata Yanga juzi Jumamosi dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Timu hiyo pia imewapiku wapinzani wao kwa kufanikiwa kupiga pasi 231 dhidi ya 174 za Waarabu hao.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kipindi cha kwanza Yanga iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 ilipiga pasi 126 huku tano zikipotea. Kipindi cha pili ikapiga pasi zenye macho 70 na kupoteza tisa.
Al Ahly walipiga pasi 94 zenye macho katika kipindi cha kwanza huku wakipoteza sita na kipindi cha pili walipiga pasi safi 67 na kupoteza saba.
Mashuti;
Yanga iliongoza pia katika kupiga mashuti baada ya kupiga mara 15 katika muda wote wa mchezo huku Al Ahly wakipiga mashuti manne tu katika lango la wapinzani wao.
Kipindi cha kwanza, wenyeji walipiga mashuti matano yaliyolenga goli huku matano mengine yakipita pembeni ya goli, Al Ahly walipiga mashuti mawili tu ambayo yote yalilenga goli.
Kipindi cha pili Yanga ilipiga mashuti matano ambayo mawili pekee ndiyo yaliyolenga lango ambapo shuti la mwisho lililopigwa na Emmanuel Okwi dakika ya 82 na kupanguliwa na kipa Sherif Ahmed ndilo lililosababisha kona iliyozaa bao lililofungwa kwa kichwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Al Ahly walipiga mashuti mawili tu katika kipindi hicho.
Safu ya ulinzi ya Yanga kwa mara ya kwanza ilionyesha ipo sawa kwa kupunguza makosa yao ya kila siku, ilifanikiwa kuwadhibiti vilivyo washambuliaji wa Al Ahly wakiwamo Mohammed Nagy ‘Gedo’ na Amr Gamaal ambao ni hatari kwa mipira ya vichwa.
Mabeki wa Yanga walifanikiwa kupiga vichwa kuwazidi ujanja mastraika wa Al Ahly kwa kufanikiwa kupiga vichwa mipira sita katika kipindi cha kwanza wakishindwa minne pekee wakati katika kipindi cha pili, walipiga mipira minne na kushindwa miwili pekee.
Kwenye lango la Ahly Yanga ilifanikiwa kupiga mipira ya vichwa mara tatu huku kimoja pekee kikizalisha bao.
Kona;
Yanga ilitawala kwa kupiga kona 12 katika muda wote wa mchezo huku Al Ahly wakipiga kona mara manne tu. Kipindi cha kwanza, Yanga ilipata kona nane huku Al Ahly wakipata moja tu. Kipindi cha pili wenyeji walipata kona nne na Al Ahly walipata tatu.
SOURCE: MWANASPOTI