Bodi ya Maji bonde la Wami Ruvu wametoa msaada wa mifuko ya Saruji 50 kwa Shule ya Msingi Kidunda iliyopo kata ya Mkulazi Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasy amesema msaada wa mifuko hiyo ni kutekeleza agizo la Waziri wa Maji Juma Aweso alilotoa alipofika katika Kijiji hicho kukagua eneo litakalojengwa Bwawa la Maji la Kidunda.
Mhandisi Mmasy amesema Bodi hiyo ilipewa maagizo ya kutoa mifuko ya Saruji 50 na DAWASA mifuko 50 ili kuunga mkono juhudi za Wananchi wa eneo hilo na kuendelea kulinda vyanzo vya Maji ambavyo vimekuwa tegemezi kwa wakazi wa Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam
” Mheshimiwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso aliona kuna umuhimu wa sisi kusaidia shule hii mifuko hii 50 ya Saruji hivyo naamini itasaidi katika Ujenzi wa Miundombinu mbalimbali ya shule hii na kupunguza adha wanazopata wanafunzi”amesema Mmasy.
Akipokea mifuko hiyo Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini mashariki Hamis Taletale maarufu kama Babu tale amemshukuru Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwa kutimiza ahadi yake kupitia Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu.
Babu tale amesema kupatikana kwa mifuko hiyo imeleta chachu kwa wananchi kuendelea kuiamini Serikali ya awamu ya sita huku akimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo Hilo ikiwemo kupatikana kwa kituo cha afya Mkulazi .
Seba Johnson ni mwaliku mkuu wa shule ya Msingi Kidunda amesema shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi za miundombinu ikiwemo uhaba wa matundu ya vyoo ambapo kwa saaa kuna zaidi ya wanafunzi mia tatu huku kukiwa na matundu ya vyoo 6 na mahitaji matundu 16 ikiwa na upungufu wa matundu 10 hivyo msaada huo utasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.