Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Afya, na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora zimeagizwa kufanyia kazi changamoto zinazowakabili wauguzi nchini ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa Mei 12, 2024 jijini Tanga na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani.
Dkt. Biteko amesema wauguzi ni asilimia 60 ya watumishi katika sekta ya afya na mchango wa huduma zao katika sekta hiyo ni asilimia 80 na hivyo ni muhimu wanataaluma kuthaminiwa na kuaminiwa pamoja na kupewa dhamana ya madaraka kama ilivyo kwa taaluma nyingine.
“Uuguzi ni taaluma muhimu hatuwezi kumfanya kuwa daraja la pili katika utendaji kazi ikiwemo nafasi za uongozi. Wizara ya Afya liangalieni hili ndani ya mwaka huu wa fedha unaoisha Juni, 30 jambo hili liwe limefanyiwa kazi”, amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza kuwa changamoto za wauguzi zimewasilishwa kwa viongozi wakuu wa kitaifa akiwemo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Isdor Mpango ambao kwa nyakati tofauti wametoa maelekezo ya kufuatiliwa na kupatiwa suluhu.
“Viongozi wametoa maelekezo juu ya suala hili, mimi siwezi kutoa maelekezo tofauti bali kufuatilia utekelezaji wa maelekezo hayo na bahati nzuri nasimamia uratibu wa shughuli za Serikali na hili ni mojawapo”, amesisitiza.
“Kama inawezekana wambie inawezekana na kama haiwezekani wambie haiwezekani ili suala hilo limalizike” ameongeza Dkt. Biteko.
Amefafanua kuwa tayari amewasiliana na Utumishi ambao wako tayari kulifanyia kazi suala la wauguzi kujiendeleza kitaaluma kwa vile wanakwenda kusoma si kwa faida yao binafsi bali wananchi wanaokwenda kupata huduma.
Aidha, Dkt. Biteko amebainisha kuwa Serikali inafanyakazi kubwa ya kuimarisha miundombinu na imeendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha sekta ya afya huku akitolea mfano ujenzi wa nyumba za watumishi wa sekta hiyo ambapo kutoka mwaka 2021 hadi 2023 jumla ya nyumba 308 zimejengwa, vituo vya afya vya upasuaji kutoka 340 hadi 523 kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na hivyo ni muhimu kuangalia uwekezaji huo katika eneo la raslimali watu.
Amesema pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo wauguzi waendelee kuhimizana katika kutimiza wajibu wao huku akiwaasa Watanzania kuwatia moyo wauguzi wakati wakiwa wanatekeleza majukumu yao.
Halikadhalika, Dkt. Biteko amewapongeza wakinamama wote duniani kwa mchango wao muhimu katika kuendeleza na kukuza ustawi wa jamii, ikiwa ni Siku ya Mama Duniani.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amewahimiza wauguzi kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuboresha huduma za afya nchini.
Naye, Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Alexander Baluhya amesema kuwa wauguzi hao wakiwa mkoani Tanga wamefanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuchangia damu, kuhamasisha wananchi kufanya vipimo kwa hiari ikiwemo VVU, tezi dume, shinikizo la damu na magonjwa yasiyoambukiza.
Katika hatua nyingine, wauguzi hao wamekula kiapo cha uaminifu ikiwa ni kujikumbusha sheria kanuni na taratibu za kutoa huduma bora kwa wananchi.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Wauguzi Duniani yamehudhuriwa na wauguzi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara yameongozwa na kaulimbiu inayosema “Wauguzi; sauti inayoongoza, wekeza katika uuguzi, heshimu haki linda afya”