Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kuna changamoto ya upungufu wa umeme katika vituo vya uzalishaji umeme nchini unaochangiwa na ongezeko la mahitaji ya umeme kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi, upungufu wa maji kwenye vituo vya kufua umeme unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na matengenezo yanaoendelea kwenye visima vya gesi asilia na mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia.
“Kufuatia hali hiyo, baadhi ya maeneo nchini yamekuwa yanakosa huduma ya meme kwa nyakati tofauti, Shirika limepokea na tayari limeanza kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Nishati na tayari jitihada mahususi za utekelezaji za kukabiliana na changamoto hii zimeanza, kwa kuharakisha matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme na matengenezo ya visima vya gesi asilia kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)”
“Ni matarajio yetu kuwa ndani ya mwezi Oktoba kukamilika kwa matengenezo hayo kutawezesha kupata nafuu ya makali ya upungufu wa umeme na ndani ya miezi sita kuhakikisha tunaondokana na kadhia hii ya upungufu wa umeme”
“Vilevile, Shirika linaendelea kukamilisha utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2115 ambao mpaka sasa umefikia asilimia 92, mradi huu utakapokamilika na kuingizwa kwenye gridi ya taifa utachangia kuimarika kwa hali ya umeme chini kwa kiasi kikubwa”
“Shirika linawashukuru Wateja wake na kuwaomba kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito na kwamba Shirika litaendelea kutoa taarifa za upatikanaji wa umeme kwa kadri hali itavyozidi kuimarika”