MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) kuendelea kutoa Elimu kwa Wananchi juu ya matumizi ya mfumo wa maji taka kwa wakazi wa Jiji hilo ili kuondoa changamoto zilizopo zikiwemo za uzibaji kutokana na kutupwa takataka ngumu.
Ummy ambaye pia ni Waziri wa Afya alitoa kauli hiyo jana wakati wa ziara yake ya kutembelea mamlaka hiyo ilikwenda sambamba na kutembelea mfumo wa maji taka kwenye baadhi ya maeneo Jijini humo.
Hatua hiyo ni baada ya kupata malalamiko ya baadhi ya Wananchi kwamba chemba zinafurika na maji machafu na kusambaa barabarani na hivyo kusababisha kero na usumbufu kwa wananchi na wakazi wa maeneo husika.
Aliyasema hayo jana wakati alipofanya ziara ya kutembelea Mamlaka hiyo na kuzungumza na Mkurugenzi wa Tanga Uwasa ikiwemo kufanya ziara ya kutembelea maeneo ya Ngamiani Kati na Usagara ili kuweza kujionea mfumo wa maji taka.
Akiwa kwenye ziara hiyo Mbunge Ummy alisema Tanga Uwasa walimueleza kwamba changamoto hiyo inasababishwa na wananchi wenyewe kutokana na kuweka nguo,matambara kwenye chemba wakati wanaoga hivyo kuchangia kwa asilimia kubwa kuziba.
“Tatizo ambalo nimeambiwa na Tanga Uwasa ni kwamba mmekuwa mkiweka vitu kwenye chemba yakiwemo matambara,mashuka,mablangeti na mapapasi ambavyo vinasababisha kuzuia maji yasipite kubwa acheni kufanya hivyo kwani hii inasababisha kupelekea kusababisha wakati mwengine mifumo ya maji taka kuziba”Alisema
“Kikubwa nimewataka waendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mfumo wa maji taka lakini nimefurahi kuona sasa mmenunua mtambo mkubwa wa kuzibua maji taka”– Alisema Mbunge Ummy Mwalimu.
Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo,Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga(Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly aliomba wananchi wa Jiji la Tanga walio karibu na mtandao wa maji taka wakiona chemba imefurika watoe taarifa kwao ili waweze kuona namna ya kuishughulikia.
Alisema kwamba hivi sasa wamepata mwarobaini wa changamoto hiyo baada ya kupata mtambo mkubwa wa kuzibua maeneo yaliyokuwa yameziba kwenye mtandoa hivyo kero yote ya maji taka inakwenda kuondolewa.
Hata hivyo aliwataka wananchi kutokuweka Taka ngumu kwenye mfumo wa maji taka kwa sababu hiyo ndio inasababisha mfumo uzibe na hatimaye maji kufurika kwenye chemba na yaonekana barabarani.