Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza Alhamisi kuwa zaidi ya watu 12,000 wameuawa tangu mapigano kati ya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) yazuke katikati ya Aprili.
Kwenye ripoti yake mpya OCHA ilisema Mradi wa Maeneo ya Migogoro ya Kijeshi na Takwimu za Matukio (ACLED) unakadiria kuwa takriban watu 12,190 wameuawa tangu mapigano hayo yazuke.
Ikilinganishwa na wiki nne zilizopita, ACLED ilirekodi vita hivyo kupungua kwa asilimia 10 huku milipuko na vurugu za maeneo ya mbali nchini Sudan zikipungua kwa asilimia 38. Halikadhalika OCHA ilisema takriban watu milioni 5.3 wamekimbia makazi yao ndani ya Sudan na kuongeza kuwa takriban watu milioni 1.3 walivuka mipaka na kwenda nchi jirani, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.
Sudan imekuwa ikishuhudia mapigano makali kati ya SAF na RSF katika mji mkuu Khartoum na maeneo mengine tangu Aprili 15.