Shirika la Afya duniani (WHO) limetangaza mpango wa muda kuhusu jinsi nchi zitakavyopewa chanjo za corona mwaka huu, huku Tanzania na Burundi zikiwa hazimo.
WHO limasema kuwa chanjo hizo ambazo ni dozi milioni 336 za AstraZeneca/Oxford na Pfizer-BioNTech, zitatolewa kwa muhula wa kwanza na wa pili ya mwaka 2021.
Kwa mujibu was WHO katika awamu hii, nchi zitapewa kwa sawa na 3.3% ya watu katika kila nchi katika mpango huu, kulingana na malengo ya shirikisho chanjo duniani GAVI ya utoaji wa chanjo kwa 3% ya wakazi wa dunia katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka 2021.
Katika orodha ya awali kuhusu mpangilio wa nchi zitakazopata chanjo katika eneo la Afrika Mshariki Tanzania na Burundi hazimo.
Nchi nyingine za Afrika ambazo hazimo katika orodha ya upokeaji wa chanjo ni pamoja na, Equatorial Guinea, Eritrea, Gabon, Lesotho, Madagascar na Ushelisheli
Shirika hilo la afya duniani linasema kuwa nchi ambazo hazimo katika orodha yake ya kupewa chanjo ya corona kwasababu “zilijinunulia chanjo zake zenyewe, hazikuomba chanjo, au hazijawekwa bado katika orodha ya nchi zitakazopewa chanjo “.