Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kwa mwaka 2024 Shirika la Fedha Duniani (IMF) limesema kuwa Tanzania inatarajia kuwa kati ya nchi 20 zenye uchumi unaokuwa kwa kasi duniani.
Rais Samia amesema hiyo ni fursa kwa wawekezaji wa Norway nchini Tanzania kwani pia ina mazingira mazuri ya kisiasa, kijiografia na kiuchumi. Wakati akihutubia Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya nchi hizo mbili, uliofanyika jijini Oslo, Rais Samia amebainisha zipo kampuni kadhaa za Norway zilizotumia fursa hiyo vizuri kwa uchumi wa Tanzania.
Aidha, Rais Samia amesema kisiasa Tanzania ina amani chini ya demokrasia imara ya mfumo wa vyama vingi wenye kuzingatia tunu za utawala bora, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.
Kwa upande wa kijiografia, Rais Samia amesema Tanzania inafaa kwa uwekezaji kwani ina Bandari ya Dar es Salaam katika Bahari ya Hindi, inayohudumia mataifa manane ya Afrika inayopakana nayo.
Kiuchumi Tanzania ina sera nzuri na imara za kiuchumi na kifedha huku ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) ukirejea kwenye 5.2% kwa mwaka. Unatarajiwa kufikia zaidi ya 6% kwa mwaka ujao kama ilivyokuwa kabla ya COVID 19.