Tanzania imetajwa kuwa kinara wa zoezi la anuani za makazi katika Bara la Afrika kwa kufanikisha utekelezaji wake kwa asilimia 95.
Mafanikio hayo yametajwa na Mratibu wa zoezi la anuani za makazi Kitaifa Bw. Jampion Mbugi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Watendaji Kata, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Wakusanyaji taarifa kuhusu utekelezaji wa mfumo za anuani za makazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema kufanikiwa kwa zoezi hilo kumechangiwa na Wakuu wa Mikoa kutekeleza vyema wajibu wao kwa kushirikiana na kwa karibu na Watendaji na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa.
Kwa Upande wake Afisa Tawala Wilaya ya Morogoro Hillary Sagala, akisisitiza Jamii kutoharibu alama za anuani za makazi, ambapo baadhi ya maeneo vimeondolewa hali ambayo inakwamisha jitihada za Serikali.
Amesema Serikali inaendelea kutoa Elimu ya kuongeza uelewa kwa jamii namna ya kuthamini miundombinu hiyo ambayo imetumia kiasi kikubwa cha fedha kukamilisha utekelezaji wake.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamehusisha washiriki 1200 wanaotarajiwa kufanya uhakiki wa anuani za makazi baada ya mafunzo kwa siku 14.