Timu mbili zinazoiwakilisha kanda ya Afrika Mashariki na Kati kwenye michuano ya kandanda ya mataifa barani Afrika, AFCON, zinateremka dimbani baadaye leo kwa mechi za kwanza za hatua ya makundi zote zikiwa kundi F.
Kikosi cha Taifa Stars ya Tanzania, kitakuwa na miadi na moja ya miamba ya soka barani Afrika, timu ya taifa ya Morocco.
Taifa Stars inayoshiriki michuano ya AFCON kwa mara ya tatu itakuwa na kibarua kigumu cha kuwashinda ´Simba wa Milima ya Atlas´, walioandika historia mwaka 2022 kwa kuwa timu ya kwanza barani Afrika kutinga nusu fainali ya kombe la dunia.
Morocco ina wachezaji mahiri kama Achraf Hakimi lakini inatajwa vilevile kwamba kikosi cha Stars nacho kinao nyota walio na ari ya kuonesha kandanda safi kwenye uga wa bara zima.
Timu nyingine ya kanda hiyo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo itapimana ubavu na Zambia katika mchezo mwingine wa kundi F.
Zambia ilibeba kombe la AFCON mwaka 2012. Kongo inayoshiriki michuano ya AFCON kwa mara ya 20 nayo ina historia nzuri kwani ilikwishalitwaa taji hilo mara mbili mnamo mwaka 1968 na 1974.
Wakaazi wa Afrika Mashariki na Kati bila shaka wataketi mbele ya runinga zao kutizama timu gani kati ya Kongo au Tanzania itakayowatoa kimasomaso.