Mkutano wa Sita (6) wa Taasisi inayosimamia Ulinzi na Usalama wa Usafiri wa Anga Afrika Mashariki (CASSOA) unatarajia kufanyika kuanzia tarehe 15 hadi 16 Mei 2024 , katika Hoteli ya Verde visiwani Zanzibar.
Mkutano huo utawakutanisha wadau muhimu wa Usafiri wa Anga ikiwa ni pamoja na makampuni ya ndege, viwanja vya ndege, wasimamizi na wadau wa usalama katika sekta ya anga kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo pia wajumbe watajadili maswala ya utunzaji wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Hamza S. Johari amesema mikutano ya EAC Aviation ilianzishwa na Bodi ya EAC-CASSOA kama njia ya kuongeza uelewa juu ya maswala yanayoathiri Usalama wa Usafiri wa Anga katika kanda yetu wa Africa Mashariki na Duniani kwa ujumla.
Amesema malengo ya Mkutano wa Sita (6) wa EAC -CASSOA ni kuchunguza na kurejesha upya tasnia ya anga na kurudisha imani ya watumiaji, kuongeza uelewa wa fursa zinazohusiana na ubunifu wa sasa wa anga, kujadili masuala endelevu ya mazingira katika anga na Kubadilishana maarifa
Amesema kauli mbiu ya Mkutano wa Sita (6) wa EAC wa Usafiri wa Anga ni “Hatima ya Usafiri wa Anga: Kudumisha mifumo ya anga iliyo imara, endelevu, ya ubunifu, salama na yenye usalama.”
Pia amewaomba wadau wote wa Usafiri wa anga kutembelea tovuti ya CASSOA ili kuweza kujisajili ili waweze kushiriki kimamilifu katika mkutano huu ambao pia ni fursa ya kuendelea kuitangaza nchi yetu pamoja na vivutio vyake.