Tanzania na Rwanda zimekubaliana kuweka mazingira bora yatakayosaidia kuongeza ufanisi wa matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni moja ya njia za kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Kigali, nchini Rwanda pamoja na Waziri mwenza wa Mambo ya Nje wa Rwanda Mhe. Dkt. Vincent Biruta.
Rwanda imeongeza wigo wa matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya asilimia 80 kwa usafirishaji wa mizigo yake.
Mbali na usafirishaji, Waziri Makamba na Waziri Biruta wamejadili masuala mengine ya kipaumbele kwa nchi hizi mbili kushirikiana ikiwemo Nishati, Kilimo na Teknolojia.
Waziri Makamba yupo Rwanda kwa ziara ya kikazi ya siku tatu inayolenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hiyo katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ikiwemo usafirishaji.