Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kupunguza matumizi ya pombe kwa kuwa imekuwa sababu ya kuongezeka tatizo la magonjwa yasiyoambukiza, ambapo amesema takwimu zinaonesha Tanzania ni nchi ya tatu kwa matumizi ya pombe Barani Afrika ikiongozwa na Uganda.
“Hatusemi msinywe pombe, lakini tunasema mpunguze unywaji wa pombe kupita kiasi, takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha Tanzania Watu kuanzia umri wa miaka 15 na kuendelea kwa mwaka tunakunywa Lita 10.4 za pombe, kiasi cha pombe kinachonywewa Nchi nzima, kikagawanywa kwa idadi ya Watanzania miaka 15 na kuendelea kila Mtu Mwanangu ni sawasawa tunatandika kwa mwezi Lita 1 kwa mwaka Lita 10.4, tupo nafasi ya tatu Afrika baada ya Uganda anafuata Shelisheli halafu sisi, Prof. Janabi anasemaga bia moja mbili ukimaliza unaangalia mpira wako unaondoka, sio uweke mzigo wa bia hapana”
Waziri Ummy ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati akizindua kampeni ya kuelimisha jamii juu ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo katika hatua nyingine amesema ugonjwa wa Saratani umeongezeka kwa kasi mwaka 2020 ambapo umeonesha vifo vipya zaidi ya elfu 40 ukiongozwa na Saratani ya Mlango wa Kizazi.
“Tusipochukua tahadhari ugonjwa wa Saratani unaweza kufikia vifo mil. moja ifikapo 2050, Saratani inachangia kwa asilimia 33 ya vifo vyote nchini Tanzania”