Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ Troika).
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) alipokutana na Mkurugenzi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Prof. Kula Ishmael Theletsane katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, Balozi Mbarouk amemhakikishia Prof. Theletsane kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Sekretarieti ya SADC katika kuhakikisha kuwa taasisi hiyo inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na ufasaha.
Viongozi hao wamezungumzia pia mipango ya uendelezwaji wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha Kanda cha (SADC-RCTC) ambacho Tanzania ni mwenyeji wake. Mipango hiyo ni pamoja na mkakati wa kukifanya kituo hicho kuwa Kituo cha Umahiri pamoja na kupata watumishi na rasilimali kwa ajili ya uendeshaji wa kituo hicho.
Kwa upande wake Prof. Theletsane ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano ambao imeutoa katika kuanzisha kituo hicho na kueleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika uendelezwaji wake. “Tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuendesha kituo kwa ufanisi, nasi pia tunaahidi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama vinaimarika kikanda,” alisema Prof. Theletsane.