Tanzania imechaguliwa tena kuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC) kwa muda wa miaka miwili kuanzia Aprili mosi mwaka huu.
PSC ilitoa tangazo hili Alhamisi kupitia X, zamani Twitter, na pia kuwataja wajumbe wengine tisa waliochaguliwa kuwa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea ya Ikweta, Uganda, Misri, Angola, Botswana, Cote d’Ivoire, Sierra Leone na Gambia.
PSC ni chombo cha kudumu cha kufanya maamuzi cha AU kwa ajili ya kuzuia, kusimamia na kutatua migogoro.
Baada ya Tanzania kuchaguliwa tena, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania January Makamba, alituma tena kwenye mtandao wa X taarifa za Umoja wa Afrika na kuwashukuru walioipigia kura Tanzania.