Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo amesema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, Tanzania inaendelea kupaa kwenye viwango katika kuvutia na kupata Wawekezaji wengi ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Mhe. Nyongo amesema hayo wakati akizindua Idara ya Magonjwa yasiyoambukiza ya Hospitali ya Rufaa ya Kisasa ya Shifaa Pan African Hospitals Limited, jijini Dar es Salaam.
Amesema Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeendelea kukaribisha, kuhamasisha na kuvutia uwekezaji kwenye sekta zote ikiwemo sekta muhimu ya Afya. Pia, ameendelea kuwakaribisha Wageni na kuwahamasisha Watanzania kuwekeza Tanzania.
Mkurugenzi wa Idara ya Uhamasishaji Uwekezaji, TIC, Bw. John Mnali amesema wanaendelea kutoa huduma bora kwa Wawekezaji wote hususan Wawekezaji wenye miradi ya kimkakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shifaa Pan African Hospitals Limited, Bw. Bashir Haroon amesema wameanzisha mradi huo wa Hospitali hapa nchini, ili kuepusha gharama nyingi zinazotokana na matibabu kwa Wagonjwa wengi kupelekwa kutibiwa nje ya nchi.