Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amemuwakilisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Kongamano la 10 la Maji Duniani (10th World Water Forum) linalofanyika Bali nchini Indonesia tarehe 19-25 Mei 2024.
Katika Mkutano wa Ngazi za Juu (High-Level Meeting), ulioongozwa na Mheshimiwa Joko Widodo, Rais wa Indonesia pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa m
balimbali Duniani, Tanzania imeithibitishia Dunia kuhusu utashi na uongozi wa kisiasa katika kutatua matatizo ya maji.
Baada ya Waziri wa Maji kuwasilisha kauli na tamko la Tanzania kwa niaba ya Mhe Rais Samia lililoelezea utekelezaji na mikakati inayoakisi kauli mbiu ya kongamano ya Maji kwa ustawi wa pamoja, Mataifa mbalimbali yameipongeza Tanzania kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika na mikakati iliyojiwekea hususani katika eneo la kufikisha huduma ya Maji Vijijini.
Akiwasilisha tamko la nchi ya Tanzania Aweso amesema Kaulimbiu ya Kongamano hilo inayosema “maji kwa ustawi wa pamoja (water for shared prosperity),” inapambanua umuhimu wa maji katika utu, maisha na maendeleo katika nyanja za afya, elimu, ajira, amani, utulivu wa kijamii na hifadhi ya mazingira.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso amebainisha umuhimu wa mdahalo wa kitaifa na kimataifa kuhusu maji na kuiweka agenda ya maji katika vipaumbele vya kitaifa na mikutano ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa na World Economic Forum. “Wakati wa maamuzi ni leo, wakati wa uongozi wa kisiasa kutatua matatizo ya maji ni leo” amesema Aweso.