Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kurejesha amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ukanda wa Maziwa Makuu.
Pongezi hizo zimetolewa Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Mhe. Balozi Huang alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) Jijini Dar es Salaam
“Umoja wa Mataifa tunaipongeza Tanzania kwa kulinda misingi ya amani na kuwa mstari wa mbele katika kurejesha amani na usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu,” alisema Balozi Huang.
Mhe. Huang ameongeza kuwa ni wakati muafaka kwa viongozi wa Ukanda wa Maziwa Makuu kusaidia kuhakikisha kuwa amani inapatikana Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kuliwezesha taifa hilo kusonga mbele kiuchumi na kisiasa.
Kwa upande wake Waziri Makamba ameupongeza Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kudumisha amani katika ukanda wa Maziwa Makuu kwani ndiyo njia itakayosaidia kuwalinda raia na kukuza uchumi katika ukanda huo.
“Tanzania chini ya uongozi imara wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaamini amani ndio msingi pekee wa maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Makamba.