Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imeruhusu tena vibali vya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) vya kuendesha safari za ndege za abiria kati ya Nairobi na Dar es salaam chini ya vifungu vya Haki za Uhuru wa Trafiki namba tatu na nne na imetengua uamuzi wake wa jana.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema wametoa ruhusa hiyo baada ya uamuzi wa Mamlaka ya Anga ya Jamhuri ya Kenya kukubali ombi la Tanzania la Kenya kusafirisha mizigo yao yote kwa kutumia Kampuni ya Air Tanzania kuanzia leo January 16,2024 kwa kuzingatia Haki za Trafiki nambari tano kati ya Nairobi na Nchi za dunia ya tatu.
Itakumbukwa jana baada ya TCAA kutangaza zuio la KQ kutua Tanzania, saa chache baadaye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alinukuliwa akisema amefanya mazungumzo na Waziri mwenzake anayeshughulikia masuala ya kigeni Nchini Kenya, Musalia Mudavadi na wamekubaliana kumaliza sakata hilo ndani ya siku tatu.