Serikali ya Tanzania imesaini mkataba maalum kwa ajili ya mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), unaotarajia kufanyika jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kuanzia tarehe 9 hadi 13 Septemba 2024.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amebaibisha hayo (04.07.2024) jijini Dar es Salaam, baada ya kusaini mkataba huo na Katibu Mkuu Msaidizi wa OACPS Bi. Cristelle Pratt na kubainisha kuwa mkutano huo utaleta nchi wanachama 79 ambao ni mawaziri na wataalamu wanaoshughulika na Sekta ya Uvuvi pamoja na Uchumi Buluu.
Prof. Shemdoe amesema mkutano huo utajadili namna wananchi wanavyoweza kunufaika na Bahari ya Hindi kupitia uchumi wa buluu, sekta ya uvuvi, usafirishaji, kilimo cha mwani, utunzaji wa bahari na kudhibiti uvuvi haramu.
Mkutano wa kusaini mkataba huo maalum umehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede, Mhe. Balozi Jestas Nyamanga Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya pamoja na kamati ya maandalizi ya mkutano kutoka wizarani.