Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini Mkataba Mpya wa Ubia baina yake na Nchi Wanachama wa Caribbean, Afrika na Pacific (OACPS) kwa upande mmoja na Umoja wa Ulaya (EU) na Nchi Wanachama wake, kwa upande mwingine.
Mkataba huo umesainiwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga kwa niaba ya Serikali ya Tanzania katika Makao Makuu ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Nchi za OACPS tarehe 19 Desemba 2023.
Mkataba huu unachukua nafasi ya Mkataba wa Ubia wa Cotonou uliosainiwa mwaka 2000, ambao utafikia ukomo wake tarehe 31 Desemba 2023. Hivyo, kuanzia tarehe 1 Januari 2024, Mkataba huu mpya uliopewa jina la Samoa ndiyo utakuwa msingi wa kisera na kisheria kuongoza ushirikiano na ubia na EU kwa kipindi kijacho.
Maeneo muhimu ya ushirikiano katika Mkataba huu ni pamoja na ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu; biashara na uwekezaji; utunzaji wa mazingira na kukabaliana na athari za mabadiliko ya tabianchi; kukabiliana na matishio mapya ya amani na usalama; uhamiaji; demokrasia na haki za bianadamu.
Itakumbukwa kuwa, ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na EU ulioanza rasmi mwaka 1975, umekuwa ukijengwa katika mikataba ya ubia ambayo imekuwa ikisainiwa baina ya nchi za OACPS na EU. Ni kupitia mikataba hii ya Ubia, Tanzania imekuwa ikinufaika kwa kiasi kikubwa kwenye ushirikiano wake na EU, katika maeneo mbalimbali, ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, misaada ya maendeleo na maeneo mengine.
Kwa mfano, katika kipindi cha kuanzia mwaka 1997 mpaka mwaka 2022, Tanzania ilipokea kutoka EU uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani zaidi ya billion 3.4. Kwa upande wa biashara, mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la EU yameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo mpaka kufikia mwaka 2021 yalifikia Dola za Marekani milioni 891.5.