Tanzania imeshika nafasi ya nne barani Afrika kwa kupata asilimia 86.9 na kuwa miongoni mwa anga bora hivyo, kuwahakikishia wageni mbalimbali wanaoingia nchini kutumia anga hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Hamza Johari amesema asilimia hizo zinatokana na viwango vya usalama wa anga vinavyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
Akizungumza leo Oktoba 29, 2023 jijini Dar es Salaam kuelekea sherehe za miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo Novemba 1, 2003, Johari amesema pamoja na mambo mengine, waliandaa mbio za marathon kwa watu wa sekta ya anga pamoja na wadau wake kwa kukimbia umbali wa kilomita 5 na 10.
“Mamlaka hiyo ilianzishwa mwaka 2003, na baada ya miaka 10, ICAO ilifanya tathmini kuhusu usalama wa anga letu na kutupa asilimia 37.8 ambayo ilituweka kati ya Mataifa ambayo si salama kusafiri,” amesema Johari.
Ameeleza kuwa mwaka 2017 shirika hilo liliwapima tena na kupata asilimia 69.04 hivyo, kutambulika kuwa miongoni mwa mataifa yanye usalama wa kutosha wa kusafiri angani.
“Kutokana na matokeo hayo tulipewa zaidi ya Dola za Marekani milioni moja ili kuboresha maeneo ambayo hayapo na tunatarajia kupata nafasi nzuri zaidi katika ukaguzi ujao,” amesema.
Amebainisha kuwa kupitia juhudi za serikali wameweza kuongeza ndege hadi 13 na kuboresha viwango vya viwanja vya ndege nchini.
Alisema miaka 20 tangu mamlaka hiyo ianze kazi, wamekuwa wakitoa huduma za usafiri wa anga nchini ikiwamo Burundi na Rwanda.
Aidha Johari ametoa wito kwa wana anga wote, watumishi na watanzania kwa ujumla kujali afya zao , kuzingatia mlo na kufanya mazoezi kwani mazoezi ni tiba na ni sehemu ya afya ambayo itasaidia kuepuka magonjwa nyemelezi na kuhatarisha maisha.
Naye wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa TCAA, kwa kufanikisha majadiliano yaliyompata mwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam na kwamba tukio hilo litaboresha utendaji kazi katika Bandari na hivyo kuongeza mapato.
Komba amesema ili nchi yoyote iweze kuimarika kiuchumi inahitaji kuwa na mfumo thabiti wa usafiri ikiwemo usafiri wa anga, maji na barabara.
“Mfumo wetu wa usafiri wa anga umepanuka na kuwa na ndege 13 na kufikia viwanja vya ndege vya kawaida,” alisema.
Kwa upande wake Lugalo Mwasamola kutoka LATRA ambaye alikuwa mshindi wa pili KM 5 amesema mashindano yalikua mazuri na atajitahidi kufanya vizuri zaidi kwa mashindano yajayo.