Tanzania imeendelea kusisitiza adhma yake ya kuwa kituo kikuu cha uchimbaji madini barani Afrika, kupitia hatua zake mbalimbali za kimkakati na kiujumuishi ikiwemo sera zake zinazotoa motisha kwa wawekezaji sambamba mazingira bora ya uwekezaji.
Dk. Steven Kiruswa, Naibu Waziri wa Madini, alitangaza dhamira hiyo wakati wa majadiliano kwenye Uzinduzi wa Mkutano wa 10 Maonyesho ya Nishati na Uchimbaji yaliyofanyika kwenye kituo cha Mikutano cha Joaquim Chissano, Maputo Msumbiji hivi karibuni.
Dkt. Kiruswa alithibitisha kuwa sekta ya uchimbaji madini nchini Tanzania inapitia ukuaji wa haraka, kwa kiwango cha asilimia 10.9 kwa mwaka, na kuchangia asilimia 9.1 ya uchumi wa taifa.
Alibainisha kuwa mafanikio hayo yamechagizwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa sheria na kanuni rafiki kwa wawekezaji, huku akielezea matarajio ya Tanzania kuvutia zaidi wawekezaji katika miezi ijayo.
‘’Ukuaji huu imara wa sekta ya madini nchini Tanzania ni matokeo ya uwepo wa Sheria na Kanuni ambazo ni rafiki kwa wawekezaji na hivyo kutupa matumaini ya kutarajia wawekezaji zaidi katika kipindi kifupi kijacho,’’ alisema Kiruswa.
Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi alifungua mkutano huo wa siku mbili, uliohusisha zaidi ya washiriki 1,000 kutoka kote ulimwenguni, wakiwemo baadhi ya mawaziri wa kikanda. Dkt. Kiruswa alibainisha kuwa serikali imeridhia sera ya mauzo ya ndani, kuhakikisha ushiriki mkubwa wa Watanzania katika mnyororo wa usambazaji wa madini, kwa kusisitiza matumizi ya huduma na bidhaa za ndani miongoni mwa wadau wa sekta hiyo.
“Kwa sasa kampuni za ndani zinachangia asilimia 97 ya usambazaji wa huduma na bidhaa katika sekta ya uchimbaji, jambo ambalo serikali inajivunia sana,’’ aliongeza.
Zaidi, Dkt. Kiruswa alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeongeza majukumu kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili liweze kuitumikia zaidi sekta hiyo. Kupitia maboresho hayo, STAMICO sasa inashiriki kikamilifu kupitia ushirikiano na kampuni za kimataifa, kwa kutegemea uwezo wao wa teknolojia na mtaji.
Kupitia hatua hiyo Serikali pia inatarajia STAMICO kuwa na migodi mikubwa na ya kati, na tayari imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo 15 ya uchimbaji itakayokuwa inakodishwa kwa makampuni makubwa ya uchimbaji na wachimbaji wadogo, kuendena na Malengo ya 2030.
“STAMICO imekuwa ikitekeleza jukumu muhimu katika kusaidia wachimbaji wadogo kwa kutoa huduma za upimaji wa jiografia na uchimbaji. Wachimbaji wadogo nchini Tanzania wanaendelea kufanikiwa zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita,” Dkt. Kiruswa aliongeza.
Zaidi, alibainisha kuwa serikali imeiwezesha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuwa na teknolojia ya kisasa kwa ajili ya kuangazia nchi nzima na kupata na taarifa za wakati halisi kuhusu madini. Alisema ili kufanikisha hilo Tanzania inashirikiana na nchi nyingine za Afrika kupitia Mkakati wa pamoja wa Madini ili kuhamasisha upatikanaji wa madini ya kimkakati na muhimu, ili kuhakikisha ongezeko la thamani na kuuza bidhaa zilizochakatwa.
Alisema ili kuimarisha dhamira ya Tanzania ya kuimarisha sekta ya uchimbaji, serikali imeanzisha Kituo cha Uchakataji wa Madini mbalimbali wilaya Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Kituo hiki kitaongeza thamani ya nickeli na madini muhimu mengine.
Mwisho