Mwimbaji wa Bongofleva Haitham Kim ambaye hivi karibuni Wasanii na Wadau wengine kama Millard Ayo walianzisha kampeni ya kusaidia kuchangisha pesa kwa ajili ya matibabu yake amefariki leo katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke Jijini Dar es salaam.
BNB ambaye ni Rafiki wa Mume wa Marehemu na ambaye AyoTV ilimkuta Hospitali juzi wakisaidiana kumuuguza Haitham, ameithibitishia AyoTV na MillardAyo kuwa ni kweli Haitham amefariki leo Hospitalini hapo.
Katika mahojiano na @AyoTV_ hiyo juzi, Bryson ambaye ni Mume wa Marehemu alisema hali ya Haitham ilibadilika ghafla siku saba zilizopita akisumbuliwa na upumuaji ambapo ilianza kama homa ya kawaida lakini baadaye akawa anakosa pumzi hadi kupelekea kuwekewa mashine na kuchomwa sindano za kila siku zinazogharimu shilingi laki 7 kwa siku.