Ikiwa imepita miezi miwili tangu rais wa Fifa Sepp Blatter alipotangaza kuiacha wazi nafasi yake baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Fifa , shirikisho hilo limetangaza tarehe ya uchaguzi wake mkuu utakaofanyika kujaza nafasi ya Blatter.
Uchaguzi huo sasa utafanyika tarehe 26 mwezi Februari mwaka 2016 kwenye makao makuu ya Fifa huko nchini Uswisi na tayari watu kadhaa wameanza kutajwa kama vinara wa mbio za kumrithi kiongozi huyu ambaye amekaa muda mrefu .
Moja ya majina yanatotajwa kuongoza mbio za kurithi mikoba ya Blatter ni jina la rais wa sasa wa shirikisho la soka barani ulaya UEFA Michel Plattini ambaye amekuwa na azma ya muda mrefu ya kuwania urais wa Fifa na alilazimika kujitoa kwenye uchaguzi wa mwaka huu baada ya kutambua kuwa hana nafasi ya kushinda mbele ya Blatter .
Mgombea amnaye aliingia mpaka kwenye hatua ya mwisho ya uchaguzi wa mwaka huu Prince Ali Bin Hussein naye anatajwa kuwemo kwenye mbio hizi japo hakuna yoyote kati ya wawili hawa ambaye amethibitisha kuwania nafasi ya Urais wa Fifa .
Rais wa sasa Sepp Blatter aliwashtua wengi baada ya kutangaza kujiuzulu wadhifa wake zikiwa zimepita siku mbili tangu alipochaguliwa kwa kura nyingi katika uchaguzi ulihusisha wagombea wawili pekee .
Blatter aliamua kung’atuka kutokana na shinikizo kubwa juu ya Fifa lilitokana na kashfa ya uozo wa matumizi mabaya ya madaraka na ofisi pamoja na kashfa ya rushwa ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikifanyiwa upelelezi unaongoza na FBI toka nchini Marekani .