Ubomoaji wa nyumba 2155 zilizoko katika Bonde la Msimbazi, jijini Dar es Salaam, unatarajia kuanza leo kama ilivyotangazwa awali.
Bomoabomoa hiyo inafanyika baada ya fidia ya Sh. bilioni 52.61 kwa ajili ya kupisha mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi kutolewa kwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Miradi ya Ushirikiano na Benki ya Dunia na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Humphrey Kanyenye, amesema watu 2,155 kati ya 2,329 walioko kwenye daftari la kwanza wamekwishapokea malipo yao.
Amebainisha kuwa kituo cha mabasi ya mwendokasi (yard) kitahamishiwa Ubungo Maziwa na pia wanatarajia kujenga City Park itakayoongoza kwa ukubwa mkoani Dar es Salaam.
Kanyenye amesema lengo la kujenga mto huo ni kuzuia mafuriko yanayotokea katika eneo hilo.
Amesema ofisi ya uratibu wa mradi kwa kushirikiana na ofisi za wakurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Kinondoni zimeshatoa taarifa kuanza ubomoaji wa nyumba zilizofidiwa kuanzia leo.