Tausi Africa imezindua rasmi Manka, mfumo wa uchambuzi wa kifedha unaotumia teknolojia ya Akili Mnemba, uliobuniwa kuboresha tathmini za mikopo katika uchumi usio rasmi wa Tanzania. Mfumo huu unafanyia uchambuzi taarifa za benki na pesa za simu, likiwawezesha watoa huduma za kifedha kufanya maamuzi ya haraka na sahihi zaidi kuhusu mikopo. Kwa kupunguza muda wa tathmini za mikopo kutoka takriban saa 3 kwa mteja hadi chini ya dakika 2, Manka inalenga kuongeza ufanisi katika sekta ya kifedha na kusaidia ujumuishaji wa kifedha.
Uzinduzi huu ulifanyika Oktoba 24, 2024, katika hoteli ya Hyatt, Dar es Salaam, ukiwaleta pamoja wadau kutoka sekta ya benki na fedha ili kujadili athari zinazoweza kutokana na mfumo huu kwenye mazoea ya utoaji mikopo.
Eric Massinda, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania – Financial Sector Deepening Tanzania (FSDT), akitoa hotuba kuu katika hafla hiyo, alisema, “Manka inaashiria hatua kubwa tunazopiga kwenye tasnia ya fedha Tanzania. Kwa kutumia data na taarifa mbadala pamoja na teknolojia, mfumo huu unalenga kutatua changamoto kubwa za utoaji wa mikopo, hasa kwa watu wasio fikiwa kikamilifu na huduma za kifedha. Uwezo wa Manka wa kutoa tathmini jumuishi kuhusu uwezo wa kurejesha mkopo utaboresha upatikanaji wa fedha, na pia utawezesha ukuaji wa uchumi jumuishi. Kadri Tanzania inavyoendelea kukaribisha uhuru wa kifedha (open finance), ndipo umuhimu wa ubunifu wa kitechnolojia kama Manka unaongezeka ili kuhakikisha kwamba taasisi zinazotoa huduma za fedha zinaweza kuwahudumia wateja wao kikamilifu na kusaidia kukua kwa biashara ndogo na za kati.”
Wakati wa uzinduzi huo, Tausi Africa pia ilitangaza ushirikiano wake na Credit Info Tanzania ili kupanua wigo na athari za Manka ndani ya sekta ya kifedha. Ushirikiano huu unawawezesha makampuni yote mawili kutoa uwezo wa juu wa uchambuzi wa mikopo wa Manka kwa watoa huduma za kifedha mbalimbali, hivyo kuwawezesha kuwahudumia wateja wao kwa maarifa na suluhisho bora za kifedha. Ushirikiano huu unaonyesha dhamira ya pamoja ya kuboresha huduma za kifedha na kusaidia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Edwin Urasa, Meneja wa Nchi wa Credit Info Tanzania, aliisifia ubunifu huo, akisema, “Manka itaboresha kwa kiasikikubwa jinsi tunavyofanya tathmini za uwezekano wakutokulipa mikopo katika masoko yasiyohudumiwa vyakutosha. Zaidi ya tathmini ya uwezekano wa kutokulipamkopo, Manka itawezesha benki kuongeza idadi ya wateja nakutoa fursa ya suluhisho za kifedha zinazokidhi mahitaji ya kila mteja. Kwa kutumia Akili Mnemba, taasisi za kifedhazitaweza kufanya maamuzi ya uhakika yanayotokana na data kwa muda mfupi, kuhakikisha watu wengi wanapata mikopowanayohitaji.“
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Derick Kazimoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Africa Technologies Limited, alisema, “Manka imeundwa ili kuboresha upatikanaji wa mikopo kwa kuwawezesha watoa huduma za kifedha kuwahudumia wateja wao kwa ufanisi zaidi. Kwa kuboresha tathmini za mikopo na kutoa maarifa kuhusu tabia za wateja, Manka inaziwezesha taasisi kutoa suluhisho za kifedha haraka zaidi na kwa njia ya kibinafsi, siyo tu katika mikopo, bali pia kwenye bidhaa mbalimbali za kifedha. Zaidi ya hayo, Manka inasaidia kuwalinganisha wateja na chaguo za kifedha zinazokidhi mahitaji yao vyema zaidi, hivyo kuongeza upatikanaji wa suluhisho bora za kifedha kwenye soko. Kipaumbele chetu ni kuwawezesha watoa huduma za kifedha kukidhi mahitaji ya wateja wao, hivyo kufungua fursa kwa ujumuishaji bora wa kifedha.”
Mfumo huu unatumia Akili Mnemba kutoa uchambuzi wa kina wa hatari za mikopo na kuwatathmini awali watumiaji kutoka taasisi mbalimbali za kifedha kwa usahihi wa hali ya juu. Manka inaakisi dhamira ya Tausi ya “Kufungua upatikanaji wa fedha kwa uchumi usio rasmi wa Afrika” kwa kuchochea ujumuishaji wa kifedha na kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa biashara ndogo na za kati (SMEs).
Manka inawakilisha uwajibikaji na hekima ya kifedha, sifa zilizochochewa na jina lake kutoka kabila la Wachagga. Thamani hizi zinaakisiwa ndani ya Manka, ikitoa uchambuzi wa kifedha ulio wazi na wenye maarifa, unaowezesha maamuzi ya busara na kuweka njia ya fursa zaidi za kifedha nchini Tanzania.
Ufanisi ambao Manka inaleta kwenye tathmini za mikopo utasaidia taasisi za kifedha kuwahudumia wateja vyema zaidi huku ikipunguza hatari zinazohusiana na utoaji wa mikopo, hasa katika sekta ambazo kwa jadi hazikuhudumiwa vya kutosha.